Historia fupi
Utangulizi
Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju ilitangazwa rasmi kuwa Parokia tarehe 24 Agosti 2012 na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Tangazo hilo lilitolewa wakati wa Misa Takatifu ya upadrisho wa Padri Dominic Somola O.Carm, ambaye leo ndiye Baba Paroko wetu.
Parokia ilizaliwa kutoka Kigango cha Mt. Joseph – Bunju, kilichokuwa chini ya Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja – Boko. Inahudumiwa na Mapadri wa Shirika la Wakarmeli (O.Carm), na tangu Mei 2025 ipo katika Dekania ya Bunju, Jimbo Katoliki la Bagamoyo.
Leo Parokia yetu ni sehemu ya Imani, Faraja na Matumaini kwa takribani waamini 6,000, na inajenga Kanisa la Hija la Mama Bikira Maria.
Msimamizi wetu
Parokia yetu imewekwa chini ya usimamizi wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, ambaye sikukuu yake huadhimishwa tarehe 16 Julai kila mwaka.
Tunajitahidi kuishi karama nne za maisha ya Mama Bikira Maria, ambazo ndizo maadili ya wanaparokia wetu. Karama hizo ni:
Dira
Kutoa huduma za sala, hija na uinjilishaji wa Neno la Mungu.
Dhima
Kutoa huduma za kiroho na kimwili, kiuchumi na kijamii, na kuendeleza ustawi wa waamini ili waishi maisha ya kumpendeza Mungu na kuufikia wokovu wa milele.
Parokia kwa takwimu
Idadi ya Waumini
Mahali ilipo Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli
Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli ipo katika eneo la Bunju ‘’A’’, wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es salaam – pembezoni mwa barabara ya Dar es salaam – Bagamoyo.
Parokia yetu imepakana na shule za msingi za Bunju ’A’ na Heri Misinga, shule ya sekondari ya Bunju ‘A’, makanisa ya Sabato na KKKT – Bunju na kituo cha malezi ya watoto wenye uhitaji maalum cha Mt. Yohana XXIII.
Kiutawala, Parokia ipo katika Dekania ya Bunju, Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Hapo awali, ilikuwa sehemu ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa katika Jimbo Katoliki la Bagamoyo, lililozinduliwa rasmi tarehe 4 Mei 2025.
Safari yetu
Kutoka kusali katika darasa moja lililoazimwa katika shule ya msingi Bunju “A” hadi kuwa Kanisa la Hija
Agosti 1984
Bunju inatambuliwa rasmi kuwa kigango na kuwekwa chini ya usimamizi wa Mt. Joseph.Mwaka 1985
Waamini wanajenga kanisa dogo la miti na udongo; magogo ya mikorosho yanatumika kama viti.2 Septemba 1990
Altare iliyotumiwa na Mt. Yohana Paulo II katika Misa ya Jangwani baadaye inaletwa Bunju; inatumika hadi leo.9 Januari 2017
Ujenzi wa Kanisa la Hija unaanza rasmi.25 Agosti 2019
Kardinali Pengo anaweka jiwe la msingi la kanisa jipya.Miaka ya 1980
Familia zisizozidi 20 zinaunda jumuiya moja na kusali katika nyumba za waamini, chini ya Parokia ya Damu Takatifu ya Yesu - Tegeta.Miaka ya 1990
Kanisa la miti linabomolewa na kujengwa kanisa la matofali ya saruji. Mitaa mitano inaanzishwa, ambayo baadaye inakuwa jumuiya.10 Oktoba 2009
Mapadri Wakarmeli (O.Carm) wanaanza utume wao Bunju.24 Agosti 2012
Kigango cha Mt. Joseph kinatangazwa kuwa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli; wakati huo kina jumuiya 38.Disemba, 2027
Tunatarajia kukamilisha ujenzi na kuanza kutumia Kanisa jipya
Historia kwa kina
Mapadri wa Shirika la Wakarmeli walianza rasmi huduma zao za kitume katika Kigango cha Mt. Joseph – Bunju tarehe 10 Oktoba 2009. Tangu wakati huo, wameendelea kuhudumia waamini na kushiriki katika ukuaji wa kiroho na maendeleo ya Parokia.
Paroko wa kwanza alikuwa Padri Thomas Mtey O.Carm, aliyeiongoza Parokia tangu ilipotangazwa rasmi tarehe 24 Agosti 2012. Baadaye, alihamishiwa katika Parokia ya Mt. Yakobo Mtume – Mabwepande tarehe 7 Julai 2022, baada ya Parokia hiyo kutangazwa rasmi.
Kupitia huduma zao, Mapadri wa Shirika la Wakarmeli wanaendelea kuimarisha maisha ya sala, maadhimisho ya Sakramenti, mafundisho ya imani na shughuli mbalimbali za kichungaji, kwa kushirikiana na viongozi wa walei na waamini wote.
Kama ilivyoainishwa baadhi ya vigango hivyo vimeendelea kukua na kuwa parokia au kuhamishiwa chini ya usimamizi wa parokia nyingine. Kufikia tarehe 27 Aprili 2025, vigango vilivyokuwa chini ya Parokia ya Bunju vilikuwa vimeondolewa katika usimamizi wake. Kwa sasa, Parokia ina mipango ya kuanzisha vigango vipya katika eneo lake ili kuendeleza huduma za kichungaji.
Mapadri
- Padri Flavian Komba CSSp wa Shirika la Roho Mtakatifu (‘’Holy Ghost Fathers’’) aliyepata upadrisho tarehe 02.06.2022 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli - Bunju.
- Padri Dickson Sambala O.Carm wa Shirika la Mapadri Wakrameli (‘’Carmelite Fathers’’) aliyepata upadrisho tarehe 15.08.2023 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli - Bunju.
- Sista Eliana Rweyemamu wa Shirika la Maria Imakulata aliyepata daraja la u-sista mnamo tarehe 23.07.2022 katika Parokia ya Chikukwe, Masasi-Mtwara.
- Sista M. Rafaela Peter Kafuro wa Shirika la Masista wa Mkombozi aliyepata daraja la u-sista mnamo tarehe 15.10.2022 katika Nyumba Kuu ya Shirika (‘’Holy Redeemer House’’) - Mtwara
Kigango cha Mt. Joseph kilianzishwa na waamini wasiozidi familia 20, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa mashamba ya mkonge. Waliunda jumuiya moja na kusali pamoja katika mojawapo ya familia zao, chini ya Mwenyekiti wa kwanza, marehemu Peter Chihuyo. Waliratibu masuala yote ya kiimani wao wenyewe hadi Agosti 1984, Bunju ilipotambuliwa rasmi kuwa kigango chini ya Parokia ya Tegeta, ikiongozwa na Padri Dominico wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu.
Kutafuta mahali pa kusali
Kati ya mwaka 1980 na 1985 waamini walikwenda kusali Tegeta, na baadaye katika kituo cha sala kilichojengwa Boko. Kutokana na umbali, walianza kusali katika darasa moja lililoazimwa katika Shule ya Msingi Bunju "A". Mwaka 1985 walijenga kanisa dogo la miti na udongo, bila sakafu ya saruji, katika eneo lililotolewa na mapadri wanaohudumia kituo cha watoto wenye mahitaji maalum cha Mt. Yohana XXIII.
Imani iliyojaribiwa
Waamini wa mwanzo walikutana na upinzani, na kuna wakati majengo yao ya miti yalibomolewa. Hawakukata tamaa. Padri Dominico alihakikisha wanabaki imara kiimani, wana mahali pa kusali na wanashiriki Misa Takatifu. Miaka ya 1990, kwa majitoleo yao wenyewe, walijenga kanisa la matofali ya saruji.
Kutoka mitaa hadi jumuiya
Hadi miaka ya 1990 hapakuwa na jumuiya kama zilivyo leo. Uongozi wa kigango chini ya Katekista Walter Mrema ulianzisha mitaa mitano, ambayo baadaye ikawa jumuiya: Bunju "B" (sasa Mt. Aloyce), Chalinze Kati (Mt. Joseph), Mkoani – Burumawe (Maria wa Fatima), Makondeni (Mt. Teresia wa Mtoto Yesu) na Kilungule (Mt. Gaspar).
Kukua kwa kasi
Kukamilika kwa barabara ya lami ya Dar es Salaam – Bagamoyo na ugawaji wa viwanja vya makazi mwaka 2004–2005 kulileta waamini wengi Bunju. Kanisa lilipanuliwa mwaka 2006–2007, Misa ya pili ikaanzishwa 2008 na Misa ya watoto 2009. Kigango kilipotangazwa kuwa Parokia mwaka 2012 kilikuwa na jumuiya 38; leo zipo 101.
Waamini wa mwanzo
Tunawakumbuka kwa shukrani baadhi ya waamini wa mwanzo: Lucas Chundu, Marco Mihayo, Mathias Kaasa, familia ya Pangani, Walter Mrema (katekista), Petro Singibila ("Mzee wa Kanisa"), Emmanuel Njegere, Hillary Mwema, Mzee Malaika, Mzee Nyaunyange, Valerian Lyolo, Juliana Nyansamba, Felister Nyambuga, Victoria Nicholaus, Paulo Kamata, Evarist Nziku, Hellen Chujagi, Mwl. Yusta Mrema, +Mwl. Felicia Liheta, +Suzani Mlengwe, Mwl. Gregory Mabinza, Beata Nchuja, Ntandu Nkangaa, Mwl. Anthony Mang'enya (mwalimu wa kwaya) na wengine wengi.
